Wednesday, August 18, 2010

Sasa masikini watakopesheka’


MKONO mtupu haulambwi. Huo ni msemo na wengi wanazingatia mwingine kwamba masikini hawakopesheki. Hata hivyo, Benki ya Twiga inakataa katakata kuwa masikini hawakopesheki, na inasema kwamba wanakopesheka.

Kuna la kujifunza kutoka benki hiyo; moja kubwa likiwa ni kuthubutu kupokea kikundi cha Vicoba Deborah jina lenye maana mwanamke shujaa katika Bibilia Takatifu, wakimaanisha wao ni wanawake hodari.

Mkurugenzi wa Benki ya Twiga, Hussein Mbululo amevunja mwiko wa kutowakopesha masikini. Amewapokea baada ya kujiunga katika vikundi vya watu 30 na kuwakopesha.

Mbululo tofauti na wakurugenzi wengi wa benki lukuki za hapa nchini, ameamua kuwainua masikini kwa kuwadhamini na kuwapa mkopo wa zaidi ya Sh milioni 40 Vicoba wa Deborah ili wanunue gari Africarriers na kuanzisha mradi wa kusafirisha abiria.

Hilo ni jambo la kujivunia kwa benki yenyewe na wakurugenzi au wakuu wengine wa benki nchini, kuamua kuwafuta machozi masikini kwa kuwapokea katika vikundi vyao ili kuwainua kimaisha.

Rais Jakaya Kikwete, katika nafasi mbalimbali alizozungumza na Watanzania amekuwa akikemea tabia za taasisi za fedha kuwasahau masikini, jambo ambalo Benki ya Twiga imeamua kulitekeleza kwa kuwasaidia Vicoba wa Deborah.

Rais Kikwete amekuwa akisema wazi kuwa benki zimekuwa zikiwadharau masikini kwamba hawaaminiki, hawana cha kulipa, wala hawana dhamana na kinga na hivyo hawawezi kukopa benki.

Mkurugenzi wa Benki ya Twiga, Mbululo katika mahojiano maalumu na gazeti hili anathibitisha kuwakopesha Vicoba wa Deborah ambao watakuwa wakilipa fedha hizo kupitia mapato yanayopatikana kutokana na makusanyo yao kwenye mabasi yao mawili.

0 comments:

Post a Comment